Jumapili , 16th Apr , 2017

Timu ya Mbao FC ambayo ni miongoni mwa timu zilizo katika hatari ya kushuka daraja katika ligi kuu Tanzania Bara, baada ya kipigo cha 3-2 kutokwa kwa Simba, leo imepata faraja kama si matumaini baada ya kuibanjua Tanzania Prisons bao 1-0

Wachezaji wa Mbao FC katika moja ya mechi walizocheza Kaitaba Bukoba

Katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Nyamagana Jijini Mwanza, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa ligi kuu kutumia uwanja huo tangu mwaka 1974, Mbao wamejipatia bao lao la pekee katika dakika ya 66 ya mchezo.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani wa wastani ukiwa umeanza kwa kupooza, Prisons walijikuta wakipata pigo katika kipindi cha kwanza baada ya mshambuliaji wake Jeremiah Juma kutolewa nje wa kadi nyekundu baada ya kubainika kumpiga kiwiko mchezaji wa Mbao FC, na kulazimika kucheza pungufu kwa karibu theluthi mbili ya muda wote wa mchezo.

Kwa matokeo hayo, sasa Mbao FC imefikisha point 30 na kupanda hadi nafasi ya 12 sawa na Ndanda FC huku Prisons ikibaki katika nafasi yake ya 9 na point 31.

Timu zilizo chini ya Mbao FC ni pamoja na Ndanda FC, Toto Africans, Majimaji na JKT Ruvu inayoshikilia mkia.

Katika mchezo mwingine, Mwadui FC imeishushia Ndanda FC kipigo cha mabao 4-2 katika mchezo uliopigwa Mwadui Complex Mjini Shinyanga, na kuifanya Mwadui ifikishe point 35 na kuchumpa hadi nafasi ya 6.