Jumamosi , 17th Jun , 2017

Michuano ya mpira wa kikapu ya 'Sprite BBall kings' iliyorindima leo katika uwanja wa Harbours Club Mivinjeni-Kurasini, jijini Dar es salaam hatimaye imemalizika huku timu nane kati ya 52 zilizokuwa zikiwania milioni 15 zikiwa zimepatikana.

Mchezaji wa Flying Dribbles (aliyovalia jezi ya blue) akiminyana na mchezaji wa UDSM

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya michuano hiyo, Kamishna wa ufundi na Uendeshaji mashindano wa Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Manasseh Zablon amesema ameridhia kwa asilimia kubwa kwa timu hizo zilizofuzu kwani zimeonesha uwezo na vipaji vya hali ya juu.

Bw. Zablon amezitaja timu zilizoweza kupenya hatua ya robo fainali ni Kurasini Hits kwa kupata 'goal difference' 111, The Fighter wamepata 77, Mchenga 52, TMT 49, Osterbay 33, Flying Dribblers 33, Kigamboni Heroes 31 na mwisho ni Dream Cheaser 20.

Kamishna wa ufundi na Uendeshaji mashindano wa Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Manasseh Zablon

Pamoja na hayo Zablon amezisisitizia timu nane zilizoingia robo fainali kukutana siku ya Jumatatu ya tarehe 19 Juni;  "Timu zilizofuzu katika hatua hii, nawaomba mtoe mwakilishi wenu mmoja (Captain) kutoka kila timu ili aweze kuja kushuhudia droo ya wazi ya kupanga ratiba za mechi za hatua ya robo fainali itakayofanyika siku ya Jumatatu ndani ya studio za EATV ambapo zoezi hilo litakuwa mubashara kupitia kipindi cha 5Sports kutoka EATV pamoja na nusu saa ya kwanza ya kipindi cha The Cruise ya East Africa Radio kuanzia saa 3 kamili usiku"

                                            Wachezaji wa Osterbay wakichuana DMI siku ya leo

Kwa upande mwingine, haya ndiyo matokeo ya timu zote zilizoweza kucheza siku ya leo ambapo Mchenga team waliifunga Ukonga Warriors kwa'point' 115-63, Flying Dribblers walipata 68- 35 dhidi ya UDSM, Kigamboni Heroes wakawafunga St. Louis Montfort kwa point 71- 40, huku Ardhi university wakiichapa Heroes B kwa 60-42 na kumaliziwa mtanange huo kwa Osterbay kuichapa DMI kwa point 74-41.