Jumatatu , 20th Feb , 2017

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amesema kuwa Chelsea tayari ni mabingwa wa kombe la FA, kabla hata ya mchezo wa robo fainali atakaokutana na vinara hao, wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza.

Moja kati ya mechi zilizowakutanisha Chelsea na Man United

Manchester United itakutana na Chelsea kwenye robo fainali ya kombe la FA, mwezi Machi mwaka huu, baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Blackburn Rovers, kwenye raundi ya tano ya FA hapo jana, mabao yaliyofungwa na Zlatan Ibrahimovic na Marcus Rashford.

Lakini Mourinho, anaamini mchezo huo, utafikiriwa zaidi na Chelsea, kwa kuwa hawana mashindano mengi, kama United, inayojiandaa na mchezo wa marudiano ya Europa League, dhidi ya Saint-Etienne, wiki hii, pia ikiwa na mchezo wa fainali aya kombe la ligi dhidi ya Southampton Jumapili ijayo, na michezo ya ligi kugombea nafasi nne bora.

"Kombe la FA ni kitu ninachoamini kuwa ni muhimu kwao. Inabidi kucheza na St-Etienne (Jumatano), inanibidi kucheza fainali ya kombe la ligi, inanipasa pia bila shaka kucheza na mpinzani mwingine kwenye Europa. Inanipasa kupigania nafasi ya nne bora kwenye ligi kuu. Nina vitu vingi sana vya kufikiria." Alisema Mourinho.