Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Kocha Mkuu wa Sunderland David Moyes amejiuzulu nafasi kufuatia timu hiyo kushuka daraja kutoka ligi kuu ya soka nchini Uingereza, maarufu kama EPL.

David Moyes

Mwisho wa Paka Weusi hao kukaa kwenye ligi kuu ya EPL kwa miaka, ulijulikana tangu walipopoteza mchezo dhidi ya Bournemouth mwezi uliopita.

Moyes, mwenye umri wa miaka 54, alimfahamisha mwenyekiti Ellis Short juu ya kujiuzulu kwake kwenye mkutano uliofanyika jijini London Jumatatu.

"Nawatakia wachezaji na mrithi wangu juhudi njema kwenye ligi daraja la kwanza, ili kurejea kwenye ligi kuu ya Premier," alisema  Moyes.

Kocha huyo wa zamani wa vilabu vya Everton na Manchester United alichukua nafasi ya Sam Allardyce kwenye klabu ya Sunderland, Julai mwaka uliopita, baada ya kocha huyo kupata kazi kwenye timu ya Taifa ya Uingereza.

Sunderland ilimaliza mkiani mwa ligi kuu ya soka nchini Uingereza msimu huu, ikiwa na alama 24, baada ya kushinda mechi sita tu.