Alhamisi , 22nd Jun , 2017

Mshambuliaji wa Yanga SC Simon Msuva amesema japo kiungo Haruna Niyonzima ameacha pengo ndani ya timu, wachezaji waliobaki wataendelea kuipigana kwa juhudi ili kuziba huku mashabiki wakiamini hakuna pengo linaloonekana.

Simon Msuva na Haruna Niyonzima

Msuva amesema, kuondoka kwa Haruna kumemuachia pengo kubwa ndani ya Yanga kutokana na ushirikiano waliokuwa nao ndani na nje ya Timu lakini atajitahidi kuendeleza ushirikiano na wachezaji waliobakia ili kuhakikisha timu inaendelea kufanya vizuri.

“Katika timu lazima kuwe na mazoea, mimi Haruna nilimzoea kupitiliza na hii habari kuwa amesaini Simba SC mimi sifahamu lakini kwaupande wangu kama amesaini kweli mimi nimeumia lakini ni maisha yake yeye na familia yake lakini mimi kwa upande wangu nitajitahidi kwa sababu kuna watu wengine nipo nao pale kama wa kina Kamusoko wapo wengi tu, kwahiyo nitashirikiana nao kama nilivyoshirikiana na Haruna lakini kwaupande wangu imeniuma, ” amesema Msuva.

Msuva amesema, atamkumbuka Haruna hususani ndani ya uwanja kwani walishirikiana kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanaipa timu ubingwa misimu mitatu mfululizo.

“Haruna nitakumbuka vitu vingikutoka kwake kwani licha ya Uwanjani pia ni mtani wangu na hata yeye huko alipo anajua kabisa ameniacha mchezaji mwenzake sina raha kwani tumekuwa na ushirikiano mkubwa ndani ya timu hususani katika suala la ushauri, ni mchezaji wa kimataifa ambaye na mkubali katika soka, ” Msuva aliongeza.