Jumatatu , 22nd Dec , 2014

Kocha wa Timu ya Tanzania Prisons, David Mwamaja amesema anaamini juhudi katika mazoezi pamoja na mechi za kirafiki walizocheza zitawasaidia kuweza kufanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza Desemba 26.

Akizungumza na East Africa Radio, Mwamwaja amesema mchezo dhidi ya Coastal Union ni mgumu lakini anaamini wachezaji wake wataipatia timu hiyo pointi Tatu muhimu na kuweza kujiweka katika nafasi nzuri.

Mwamaja amesema kikosi chake kina majeruhi lakini kutokana na usajili alioufanya pamoja na benchi lake la ufundi atahakikisha anatumia wachezaji waliobakia ili kuweza kuipa timu mafanikio.

Mwamaja amesema usajili uliangalia maeneo muhimu yaliyokuwa yakihitaji msaada na alihakikisha anasajili kwa kuzingatia kiwango cha mchezaji suala linalozidi kumpa imani kuwa wachezaji hao watakuwa na manufaa kwa upande wa timu nzima.