Jumatatu , 14th Sep , 2020

Kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin, amesema kuwa sababu kubwa iliyomfanya asishangilie bao alilowafunga Mtibwa Sugar ni kutokana na heshima yake kwa mabosi wake hao wa zamani pamoja na mchango mkubwa alioupata kutoka kwa Wakata Miwa hao katika maendeleo yake ya soka.

Mzamiru Yassin(Kulia) akizungumza na Mohamed Hussein(Kushoto) katika moya ya mchezo.

Mzamiru jumamosi aliifungia Simba bao lao pekee katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

“Hadi nimefika hapa nilipo, ni kwa sababu yao na hata hivi ninavyoongea, kuna mambo mengi ya mpira napata ushauri kutoka kwao, hivyo siwezi kushangilia hata siku moja pale nitakapowafunga.

“Ni lazima ninapopata nafasi ya kufunga, nifunge kwa sababu ni sehemu ya majukumu yangu, lakini hainipi fursa ya kushangilia kwani nitakuwa naifanyia makosa makubwa nafsi yangu kutokana na jinsi uongozi na waliopo katika benchi la ufundi wanavyonisaidia hadi sasa kuona natimiza malengo yangu kisoka,” alisema.

Simba ilimsajili Mzamiru msimu wa 2016/17 akipewa mkataba wa miaka miwili sambamba na wachezaji wengine, Shiza Kichuya na Mohamed Ibrahim (kwa sasa hawapo Simba) kabla ya kuongezewa mwingine baada ya kufika ukingoni ule wa awali.