Jumamosi , 24th Jun , 2017

Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali amesema hawana wasiwasi wowote juu ya kuondoka kwa kiungo wao  Niyonzima kwa kuwa wapo wengi walishaondoka waliokuwa wazuri katika timu yao akiwamo Sunday Manara na timu iliendelea kufanya vizuri.

Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali.

Mzee Akilimali amebainisha hayo kupitia kipindi cha Kipenga kutoka East Africa Radio, wakati akihojiwa na mtangazaji Tom Chilala na kusema Niyonzima aondoke tu Yanga bila wasiwasi wowote kwani ana uhakika wa kupata mchezaji mwingine wa kuziba nafasi yake.

"Mwache aende tu, Yanga ni timu kubwa na walipita wachezaji wengi zaidi yake kama vile 'Computer' na wengine wengi ambao walikuwa wazuri lakini timu iliendelea kubaki na kufanya vizuri" alisema Akilimali.

Pamoja na hayo, Mzee Akilimali amesema endapo uongozi wa Yanga utaweza kusema umeshindwa kufanya kazi zake ipasavyo basi wamuite yeye ili waweze kukaa chini na kuzungumza wapate muafaka mzuri katika klabu yao.

"Kiongozi waliyokuwepo madarakani kwanini hawatamki kuwa sisi tumeshindwa ebu watamke basi na nina kwambia wakitamka tu leo Niyonzima atarudi" alisisitiza Mzee Akilimali. 

Sauti ya Mzee Akilimali akiwa anaongea na mtangazaji wa Kipenga kutoka East Africa Radio, Tom Chilala.