Jumatatu , 16th Oct , 2017

Nahodha wa klabu ya Mtibwa Sugar Shabaan Nditi amefunguka kuhusu bao la mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi kwenye mchezo wa jana kuwa liliiumiza timu nzima.

Nditi ameyasema hayo leo wakati timu yake ikijiandaa kurejea mkoani Morogoro baada ya jana kutoa sare dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Uhuru Dar es salaam kwa bao la dakika za nyongeza ambalo amedai liliwaumiza timu nzima.

“Kila mtu aliumia kwasababu tulikuwa tumekaribia kushinda lakini dakika za mwisho Okwi akasawazisha, kiukweli hakuna lawama kwa yoyote ila tu Okwi alitumia akili nyingi kupiga mpira wa adhabu na kufunga, anastahili pongezi”, amesema Nditi.

Aidha Nditi amesema timu yake imejiandaa kwa mechi zote ili ipate ushindi na kujiweka vizuri kwenye mbio za ubingwa japo kuwa inatokea kuna mechi wanapata sare.

Mtibwa Sugar ambayo haijapoteza mechi hadi sasa inaondoka leo mchana jijini Dar es salaam kurejea Morogoro ambako itaendelea na maandalizi ya mchezo wa raundi ya 7 nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.