Jumatatu , 18th Sep , 2017

Nyota mpya wa klabu ya Paris Saint Germain PSG Neymar jana usiku alitunishiana misuli na mchezaji mwenzake Edinson Cavani wakigombea kupiga penalti katika mchezo wa Ligue 1 dhidi ya Lyon.

Penalti hiyo ilipatikana dakika ya 79 ya mchezo ambapo nyota hao wawili kutoka Amerika Kusini walishindwa kuelewana juu ya nani apige na wakapokonyana mpira kila mmoja akitaka kupiga. Baadae Neymar alimwachia Cavani ambaye alipiga hata hivyo alikosa penalti hiyo.

Kocha wa PSG Unai Emery amesema hataingilia ugomvi huo badala yake atawaacha waelewane wenyewe nani awe na jukumu la kupiga mipira ya adhabu ndogo pamoja na penalti.

Ugomvi huo huenda umesababishwa na ushindani wa mabao ambapo nyota hao wawili wanaongoza orodha ya wafungaji katika klabu hiyo kwa msimu huu, Cavani akiwa na mabao 7 wakati Neymar ana mabao 4.