Jumatatu , 12th Apr , 2021

Kufuatia klabu ya Yanga kutoka sare ya goli 1-1 dhidi ya KMC kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Mkapa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amemtupia kijembe Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Nchemba.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Nchemba (kushoto) na Spika wa Bunge Job Ndugai

Spika Ndugai ameanzisha utani huo leo Aprili 12, 2021, bungeni kwenye kikao cha 7, mkutano wa 3 wa bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo amesema wachezaji wa Yanga SC wana njaa hivyo angalau wabunge wawachangie.

"Jana nilimtafuta Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba kwa mambo yetu haya ya bunge akaniambia Spika tafadhali niache, nikauliza sasa nakuacha kuna nini tena? akasema nina 'stress', kumbe matokeo ya juzi yamempa 'stress', pole Mhe. Nchemba na wanayanga wote," - Spika Ndugai

Spika Ndugai akaongeza kwa kusema kuwa, "Taarifa tulizonazo wachezaji wana njaa, maana wamelegea legea hivi, kwa hiyo waheshimiwa wabunge baadaye tunaweza kufanya mchango kidogo tuwasaidie Yanga."

Baada ya sare hiyo, Yanga SC imefikisha pointi 51 baada ya kucheza michezo 24 huku Azam FC wakiwa nafasi pili na pointi 47 ikiwa imecheza michezo 25 na mabingwa watetezi Simba SC wakiwa na pointi 46 wakiwa wamecheza michezo 20.
 

Tazama Video hapo chini