Jumapili , 15th Oct , 2017

Klabu ya soka ya Simba imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara raundi ya sita uliomalizika jioni hii kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Bao la kuongoza la Mtibwa limefungwa dakika ya 35 kipindi cha kwanza na mshambuliaji Stamil Mbonde na lilidumu kipindi chote cha kwanza.

Kipindi cha pili Simba iliendelea kumiliki zaidi mpira kuliko Mtibwa lakini haikusaidia kurejesha bao hilo ambapo ilibidi kusubiri hadi dakika za nyongeza ndipo mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi akafunga bao kwa mkwaju alioupiga kufuatia adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la 18 la Mtibwa Sugar.

Matokeo hayo sasa yanaifanya Simba kufikisha alama 12 baada ya michezo sita. Simba sasa imerejea kileleni kwa tofauti ya mabao na timu za Yanga, Azam FC na Mtibwa Sugar ambazo nazo zina alama 12.