Jumatano , 22nd Nov , 2017

Mchezaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amekataa kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kufanikiwa kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 6-0 ilioupata timu yake dhidi ya APOEL kwenye Ligi ya Mabingwa.

Ronaldo alipofuatwa na wanahabari baada ya mchezo huo alikataa kuongea hadi pale walipomganda zaidi lakini alisisitiza kuwa hawezi kuongea chochote na hana raha ya kufanya mahojiano na wanahabari.

“Sihitaji kuongea, sihitaji kuhojiwa juu ya lolote, nimechoshwa na nafadhaishwa na namna ambavyo mnabadilisha maneno, leo naweza kuongea jambo moja kisha mkaandika tofauti kabisa na nilichosema”, amesema Ronaldo mbele ya wanahabari waliokuwa wakimzonga kwenye uwanja wa GSP.

Hatua ya Ronaldo kugoma kuongea na wanahabari ni matokeo ya habari zilizoripotiwa hivi karibuni kuwa Ronaldo ana ugomvi na nahdha wake Sergio Ramos baada ya Ronaldo kukaririwa akisema Real Madrid haifanyi vizuri kwenye La Liga kwasababu ina wachezaji wengi ambao si wazoefu baada ya kuwauza Alvaro Morata na James Rodriquez kitu ambacho Ramos alikipinga kwa nguvu.

Baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 6-0 sasa Ronaldo ameifungia Real Madrid mabao 98 kwenye mechi 96, akimzidi mshindani wake Lionel Messi ambaye ameifungia Barcelona mabao 97 kwenye mechi 119.