Jumapili , 21st Mei , 2017

Macho na masikio ya mashabiki wa soka wa Tanzania leo yanaelekezwa Gabon kwa wawakilishi wake Serengeti Boys itakayovaana na wenzao wa Niger.

Serengeti Boys

Serengeti inahitaji kupata ushindi katika mechi hiyo ya tatu na ya mwisho ya Kundi B ili kufuzu kucheza hatua ya nusu fainali na kukata tiketi ya kushiriki fainali za michuano ya Kombe la Dunia kwa umri huo zitakazopigwa India Oktoba, mwaka huu.

Serengeti Boys wenye pointi nne wanashuka uwanjani wakiwa kileleni sambamba na Mali kutokana na kupata sare ya bila kufungana na mabingwa watetezi hao na mchezo wa pili wakiifunga Angola mabao 2-1 matokeo ambayo Mali pia iliyapata dhidi ya Niger.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime alisema jana kuwa wachezaji wake wako vizuri na wamejipanga kumaliza na ushindi ili kutimiza ndoto.