Jumatatu , 20th Feb , 2017

Mchezaji wa Kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya Royal Eagles ya nchini Afrika kusini Uhuru Seleman amefunguka na kusema mafanikio yake yamekuja baada ya yeye kutoka katika vilabu vya Tanzania na kwenda nje. 

Uhuru Seleman

 

Uhuru amesema licha ya kuchelewa kutoka katika soka la nyumbani lakini angalau yeye amepata mafanikio ambayo anajivunia kwa sasa, kama vile kuweza kumiliki nyumba zake mwenyewe binafsi, kumiliki biashara mbalimbali na kuweza kuhudumia familia yake. 

"Naweza sema mimi nimechelewa sana kutoka katika soka la nyumbani, lakini hata hivyo bado najivunia vitu kadhaa ikiwemo kuwa na makazi binafsi zaidi ya nyumba moja,  kumiliki biashara na kuhudumia familia bila kuteteleka kwa lolote lakini nikukumbushe tu kuwa kucheza Simba na Yanga siyo wote wanaopata mafanikio unayoyafikiria, mimi vitu vingi nimetimiza baada ya kutoka nje" alisema Uhuru Seleman

Mbali na hilo Uhuru Seleman amezungumzia mchezo ambao utafanyika siku ya tarehe 25 kati ya watani wa jadi Simba na Yanga.

"Kiukweli sijaziangalia timu zilivyo kwa muda mrefu sasa lakini huwa mechi ya Simba na Yanga ni ngumu kuitabiri ukiwa nje ya uwanja" alisema Uhuru Seleman 

Uhuru Seleman anasema kwa sasa yeye hachezi mpira kama mapenzi bali anacheza mpira kama kazi hivyo anaangalia maslahi na kama Simba watamuhitaji tena kuja kucheza katika klabu hiyo hana tatizo ataangalia tu maslahi yake na si kitu kingine.

"Mpira kwangu ni kazi na sichezi mpira kwa mapenzi, ikitokea Simba wananihitaji nitakwenda kukiwa na maslahi katika hilo" alisisitiza Uhuru Seleman