Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Mchezaji wa timu ya Simba SC, Mohamed Hussein amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa mwezi Mei kwa msimu wa 2016/2017.

Baadhi ya wachezaji wa Simba katika moja ya mchezo wao wa ligi

Hussein aliwashinda wachezaji Haruna Niyonzima wa Yanga na Shabani Idd wa Azam FC. 

Katika mwezi Mei kulikuwa na raundi tatu ambazo Hussein alicheza kwa dakika zote 270 na kutoa mchango mkubwa katika kuisadia timu yake kubaki katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Pia alionesha nidhamu ya hali ya juu, hivyo kutopewa onyo la aina yoyote.

Kwa kushinda tuzo hiyo, Hussein atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

Mohamed Hussein

Wachezaji wengine walioshinda tuzo za mwezi za Ligi Kuu msimu wa 2016/2017 ni John Bocco wa Azam (Agosti), Shiza Kichuya wa Simba (Septemba), Saimon Msuva wa Yanga (Oktoba) na Riphat Said wa Ndanda (Novemba).

Wengine ni Method Mwanjali wa Simba (Desemba), Juma Kaseja wa Kagera Sugar (Januari), Hassan Kabunda wa Mwadui (Februari), Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar (Machi) na Abdulrahman Musa wa Ruvu Shooting (Aprili).