Jumatano , 27th Jul , 2016

Beki na nahodha wa zamani wa klabu ya Simba, Hassan Isihaka ametamka kuwa kwa sasa hana timu ya kuichezea, hivyo kwa sasa yupo nyumbani.

Nahodha wa zamani wa klabu ya Simba, Hassan Isihaka

Isihaka ambaye alitengeneza ukuta imara akiwa Simba akishirikiana na Mganda, Juuko Murshid, ametemwa katika kikosi cha Simba ambacho kimejichimbia mkoani Morogoro chini ya kocha wake Mcameroon, Joseph Omog kikijiandaa na msimu ujao wa ligi kuu.

Beki huyo anayechipukia alisema kuwa mpaka sasa amekuwa akikaa nyumbani kutokana na kutemwa na timu yake hiyo ambapo hakuna timu yoyote ile iliyomfuata kwa nia ya kumsajili.

“Nipo nyumbani tu, sina timu yoyote ya kuichezea mara baada ya kutemwa na Simba ambapo mpaka sasa hakuna timu yoyote ile ambayo imenifuata kwa ajili ya kunisajili kwa msimu ujao".

Hata hivyo Isihaka bado hajakata tamaa kutokana na kuwa baadhi ya timu bado zinaendelea na usajili hivyo anatumaini mambo yatakaa vizuri kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

“Sijajua hatma yangu itakuwaje msimu ujao kwa sababu sina timu lakini naamini mambo yatakuja kukaa vizuri kabla ya dirisha la usajili kufungwa, timu zitakuja tu,” alisema Isihaka.