Alhamisi , 30th Oct , 2014

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatarajia kuendelea na awamu ya pili ya maboresho ya timu ya Taifa (Taifa Stars) inayojumuisha vijana wenye umri chini ya miaka miaka 23

Kikosi cha taifa stars kikiwa katika jezi ambazo zilizua utata kutokana na rangi ya jezi hizo kutoendana na rangi za bendera ya taifa

Katika awamu hii, Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij ameteua majina ya wachezaji 29 ambao watakuwa wakiingia kambini mara moja kwa mwezi siku ya Jumapili baada ya kuwakilisha timu zao kwenye mechi za ligi.

Kikosi hicho cha maboresho kitakuwa kikifanya programu maalumu za mazoezi mpaka siku ya Jumatano na kucheza mechi za kirafiki na timu za ndani au nje ya nchi.

Lengo hasa la programu hiyo ni kuwajengea uwezo vijana wenye vipaji ambao walipatikana katika awamu ya kwanza ya mpango wa maboresho mwanzoni mwa mwaka huu Tukuyu mkoani Mbeya, lakini wamekuwa hawatumiki. Pia kuwandaa vijana ili kujenga timu ya ushindani na imara ya Taifa ya muda mrefu.

TFF ina imani kubwa kuwa programu hii itakuwa na manufaa kwa soka ya Tanzania. Timu hiyo itaingia kambini kwa mara ya kwanza Desemba 9 mwaka huu katika hoteli itakayotangazwa baadaye.

Wachezaji walioteuliwa ni Aishi manula (Azam), Benedict Tinoco (Kagera Sugar), Aboubakar Ally (Coastal Union), Miraji Adam (Simba), Andrew Vicent (Mtibwa Sugar), Gadiel Mbaga (Azam), Emmanuel Semwanda (African Lyon) na Joram Mgeveke (Simba).

Edward Charles (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Kassim Simbaulanga (African Lyon), Pato Ngonyani (Yanga), Adam Salamba (Kahama), Hassan Banda (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Hashim Magoma (Stand United), Makarani Ally (Mtibwa Sugar), Said Juma (Yanga) na Said Hamis (Simba).

Aboubakary Ally Mohamed (Zanzibar), Hassan Dilunga (Yanga), Hussein Malombe (Geita Gold), Muzamir Ally (Mtibwa Sugar), Shiza Ramadhan (Mtibwa Sugar), Omari Nyenje (Ndanda SC), Kelvin Friday (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Alfred Masumbakenda (Kahama) na Simon Msuva (Yanga).

Wakati huo huo TFF yaomba wadau wa michezo kubuni jezi mpya ya timu ya taifa.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linakaribisha wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani na ugenini. Ubunifu ni lazima uzingatie rangi za bendera ya Taifa.

Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata sh. 1,000,000 (milioni moja), na mshindi wa jezi ya ugenini atapata pia sh. 1,000,000 (milioni moja)

Mkurugenzi wa mashindano wa TFF Boniface Wambura amesema ni fulsa sasa kwa wabunifu kubuni jezi hizo na vema wakabuni jezi za nyumbani na ugenini.

Ubunifu utumwe kwenye anwani ya barua pepe: [email protected] au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden Avenue. Mwisho wa kupokea designs ni Novemba 15, 2014.