Ijumaa , 17th Feb , 2017

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikito taarifa ya kifo cha Nahodha wa timu ya 94 Green Warriors, Ikongo Julius Mbaga aliyefariki dunia leo alfajiri (Februari 17, 2017) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Mchezaji huyo alijeruhiwa kwenye ajali ya gari ya timu yake iliyotokea Februari 13, 2017 Ihumwa mkoani Dodoma wakati ikiwa njiani kwenda Shinyanga kucheza mechi ya Ligi Daraja la Pili (SDL) dhidi ya Bulyanhulu FC.

Taratibu za mazishi ya Marehemu ambaye mwili wake umehamishiwa Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) ya Lugalo jijini Dar es Salaam zinafanywa na familia yake kwa kushirikiana na klabu ya 94 Green Warriors. Taarifa rasmi za mazishi zitatolewa baadaye.

Wakati huo huo TFF, limetuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya kutokana na kifo cha mchezaji wa zamani Tanzania Prisons, Young Africans na timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Geofrey Bonny wakati akiugua

Taarifa kutoka Mbeya, zilizothibitishwa na uongozi wa Mkoa zinasema kwamba mchezaji huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia leo Ijumaa Februari 17, 2017 kwenye Hospitali ya Wilaya ya Rungwe.

Katika salamu zake za rambirambi, TFF imewataka ndugu wa marehemu kuwa na uvumilivu kwa kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwa Bonny ambaye nyota yake iling’ara zaidi wakati Taifa Stars inafundishwa na Mbrazil Marcio Maximo.

Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.