Alhamisi , 17th Aug , 2017

Kamishna Ufundi na Mipango ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini Tanzania (TBF), Manaseh Zabron amefunguka na kudai upinzani uliyoonyeshwa na timu ya Mchenga BBall Stars na TMT katika game 2 fainali za Sprite BBall Kings ndivyo inastahili kuwepo.

Kamishna Ufundi na Mipango ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini Tanzania (TBF), Manaseh Zabron.

Manaseh amebainisha hayo baada ya timu ya TMT kuweza kumchapa Mchenga BBall Stars kwa pointi 87-78 katika mchezo wa 'game 2' fainali za Sprite BBall Kings zilizofanyika jana jambo ambalo wengi hawakutegemea kama timu hiyo ingeweza kuwika mbele ya Mchenga BBall Stars.

"Kiukweli mabadiliko yamekuwa makubwa katika mechi ya jana, tulitegemea watapigwa sweap leo pamoja na Jumamosi lakini tumeonyeshwa taswira ya tofauti na watu walivyokuwa wametegemea. Kwa maana hiyo fainali hizi zitakwenda mpaka 'game 4",alisema Manaseh

Pamoja na hayo, Manaseh ameendelea kwa kusema "kama walivyokuwa wanajiuliza TMT mara ya kwanza walipofungwa katika fainali hizi nayo Mchenga BBall Stars itaenda kujiulia ni jambo gani kimemtokea mpaka amepoteza mchezo, naamini watakapo kutana Jumamosi katika game 3 itakuwa mechi nzuri kwa kuwa timu zote zitaitaji zishinde ili ijiweke katika nafasi nzuri ya ushindi".

Kwa upande mwingine, Manaseh amesema angependa fainali za sprite BBall Kings ziende mpaka katika 'game 5' ili iweze kuleta radha nzuri ya mchezo wa mpira wa kikapu.

Timu ya TMT na Mchenga BBall Stars zitakutana tena tarehe 19 mwezi huu katika viwanja vya Don Bosco Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambapo mpaka sasa timu zote zimepoteza mchezo mmoja na kupata mmoja kwa kila timu.