Jumanne , 5th Sep , 2017

Nahodha wa timu ya Mabingwa wa Sprite BBall Kings 2017, Mchenga BBall Stars, Mohammed Yusuph 'Muddy' amefunguka na kudai kuwa ushindi ulikuwa wao tokea awali ila wapinzani wao TMT waliwachelewesha kukabidhiwa kikombe chao katika fainali hizo.

Nahodha wa Mchenga BBall Stars, Mohammed Yusuph 'Muddy' (kushoto) akiwa na mchezaji bora Rwahabura Munyangi

Muddy ameeleza hayo wakati akizungumza katika kipindi cha Kipenga kutoka East Africa Radio na kusema wanafurahia kuwa mabingwa wa kwanza Tanzania katika mashindano ya Sprite BBall Kings.

"Tumefurahia sana kwa kuweza kuwa mabingwa wa Sprite BBall Kings 2017 lakini tokea awali mimi kama nahodha nilisema TMT, wanachelewesha tu ila wanatambua kuwa ushindi ni wetu. 'Game' ilikuwa nzuri, tunamshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa sisi kuibuka washindi pamoja na mashabiki wa timu zote kwa sababu bila ya wao mwaka huu mashindano ya Sprite BBall Kings yasingefanikiwa lakini yameweza kufanikiwa kwa ajili yao walivyokuja kutu-support", amesema Muddy.

Pamoja na hayo, Muddy aliendelea kwa kusema "tunaomba mwakani mashindano haya yawepo tena, tutakuja kama mabingwa watetezi wa mashindano ya Sprite BBall Kings ili kuweza kutetea ubingwa wetu", amesisitiza Muddy.

Kwa upande mwingine, Muddy amewashukuru waandaji wa michuano hiyo ya Sprite BBall Kings ambao ni EATV LTD wakishirikiana na Sprite kwa kuweza kurudisha heshima ya mpira wa kikapu nchini Tanzania.