Jumapili , 15th Jan , 2017

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, aliyeiongoza timu hiyo kuchukua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, amesema moto waliouwasha kwenye kwenye michuano hiyo watauendeleza katika michuano ya ligi kuu Tanzania Bara na hakuna wa kuuzima.

Idd Nassoro Cheche

Cheche amesema moto huo waliouwasha ni wa tipa (ule wa kwenye viwanda vya mafuta) na hauwezi kuzimika huku akisema kuwa jambo kubwa lilipelekea mafanikio hayo kwa kikosi chake ni mshikamano, hali ya kujituma kwa wachezaji na kufuata maelekezo yake.

“Unajua unapokuwa binadamu na ukapata mafanikio makubwa kama haya ndani ya muda mfupi lazima uwe na furaha, nawashukuru wachezaji wangu kwa kazi kubwa waliyofanya na mshikamano na hali ya kujituma na jitihada walizozionesha, kwa hakika hivyo ndivyo vilivyotupa ubingwa,” alisema.

Kocha huyo aliyekuwa akisaidiana na Kocha wa Makipa Idd Abubakar, kufanya kazi hiyo kubwa hadi kufikia mafanikio hayo, kuanzia kwenye ligi watakuwa chini ya Kocha Mkuu mpya, Mromania Aristica Cioaba, aliyechukua mikoba ya Mhispania Zeben Hernandez, aliyesitishiwa mkataba pamoja na benchi lake zima la ufundi.