Jumapili , 15th Jan , 2017

Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amefichua siri ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu, na kusema kuwa hivi sasa wanahamishia nguvu zao zote kwenye michezo ya ligi kuu Tanzania Bara.

Nahodha wa Azam, John Bocco (Katikati) akiongoza wachezaji wenzake wakati wakiingia na kombe la jijini Dar es Salaam kutoka Zanzibar

Bocco amesema kikubwa kilichowapa ushindi ni pamoja na sapoti kutoka uongozi wao ambao uliwatimizia kila kitu walichohitaji, lakini pia ushirikiano pamoja na kuwasikiliza walimu.

“Naamini hatukuwa na papara, tuliweza kutulia, tuliweza kupata sapoti kutoka kwa viongozi wetu pamoja na mashabiki wetu na kuwasikiliza walimu wetu ndio kama hivi tunamshukuru Mungu tumeanza kidogo kupata mafanikio.” Amesema Bocco

Alisema kuwa wana furaha kubwa kutwaa taji hilo huku akiwapongeza wachezaji wenzake kwa namna walivyojituma hadi kufikia fainali na kupata mafanikio hayo.

“Kwanza tunamshukuru Mungu kwa ushindi huu ni matokeo mazuri kwetu tumeweza kutwaa Kombe la Mapinduzi, kikubwa nawaomba wachezaji wenzangu tuweze kuweka jitihada katika michezo ya Ligi Kuu ianyokuja, tuwasikilize walimu wetu nini wanachotueleza ili tuweze kufanya vizuri na hata michuano ya kimataifa,” alisema.

Naye kipa bora wa michuano hiyo, Aishi Manula, ambaye amecheza mechi zote bila kufungwa bao, amesema anajisikia faraja sana kuweza kutwaa tuzo hiyo huku akiwaambia mashabiki kuwa ubingwa huo unaamanisha kuwa wao wamerudi kwenye ubora wao na kuonyesha kama ni timu kubwa.

“Napenda kumshukuru Mungu, kwa hiki ambacho wamenipatia na pia kuishukuru timu nzima kwa ujumla kwa kuweza kucheza vizuri hasa mabeki wameweza kunilinda vizuri na tumeweza kumaliza mashindano haya bila kuruhusu bao, pia ni kitu kizuri kwa sababu hili linakuwa kombe la pili kuchukua bila kuruhusu bao, kwanza Kagame tuliweza kulichukua bila kuruhusu bao na hili la Mapinduzi kwa hiyo ni kitu kizuri,” alisema.