Jumanne , 28th Feb , 2017

Uongozi wa klabu ya Yanga umesema utamuita na kumuhoji beki wake wa kimataifa Vincent Bossou kutokana na kutoonekana kwake kwenye kikosi cha timu hiyo pamoja na kambi iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao dhidi ya Simba

Vincent Bossou

Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwassa amesema Bossou amekuwa haonekani kambini wala kwenye mechi, jambo lililofanya akosekane kwenye mechi kadhaa ikiwemo ya watani zao wa jadi ambayo ilishuhudia timu hiyo ikipigwa mabao 2-1.

Mkwassa amesema, uongozi wa klabu hiyo unatambua kuwa palikuwa na tatizo la mshahara wa mchezaji huyo kwa mwezi Januari, jambo lililosababishwa na yeye kutokuwepo nchini, lakini aliporejea mshahara wake ulikuwa tayari, lakini hadi sasa mchezaji huyo hajakwenda kuuchukua

"Bossou alikwenda kwenye AFCON ndiyo sababu mshahara ukachelewa kumfikia, lakini aliporudi, alitakiwa kwenda kusaini hundi, hatuelewi kwanini hajafanya hivyo, mshahara anaodai ni mwa mwezi mmoja pekee ambao ni Januari.... Kikosi kinaanza mazoezi kwa ajili ya mechi za ligi lakini kwa upande wake tutasubiri maoni ya walimu, halafu tutamuhoji kujua ni hatua gani achukuliwe" Amesema Mkwassa.

Charles Mkwassa

Hata hivyo bado kuna utata juu ya kilicho nyuma ya pazia kati ya beki huyo raia wa Togo na uongozi wa Yanga, maana inasemekana kuwa mchezaji huyo amegoma kucheza kutokana na madai yake ya mshahara wa miezi minne, huku klabu hiyo ikisema ni mshahara wa mwezi mmoja ambao nao upo tayari.

Bossou alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliocheza dhidi ya Ngaya ya Comoro katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika.