Alhamisi , 23rd Feb , 2017

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Simon Sirro amewaonya mashabiki wapenda fujo kukaa nyumbani na kutazama mpira wa watani wa jadi (Simba na Yanga) unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ya tarehe 25 katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam.

CP Simon Sirro

Akizungumza kwenye kipindi cha EA Breakfast leo Kamishna Sirro amewataka wazazi kuwaonya watoto wao ikiwa ni pamoja na wanawake kuwaonya waume zao kutokwenda kuangalia mchezo huo uwanjani na ikibidi wabaki nyumbani ili kuepuka mkono wa dola pale watakapokutwa na makosa ya ufanyaji fujo.

Wakati huo huo Sirro amezidi kusisitiza kwamba ulinzi uliopangwa kuwepo kuzunguka kiwanja cha mpira ni mkubwa hivyo watu waliodhamiria kuliabisha jeshi la polisi kwa kuvunja viti kama walivyofanya mchezo uliopita waendelee na mipango yao hiyo.

  "Wale waliovunja watataka kurudia tena, sasa naomba warudie tena ili niwashikishe adabu, na kama mama unampenda mwanao au wewe mke unampenda mumeo na unafahamu ni wapenda fujo ni afadhali ukamshauri aangalie mpira akiwa nyumbani asiende uwanjani akapata matatizo... Nasema nina usongo sana na watakaofanya vurugu". Alisisitiza Kamishna Sirro.

Huyu hapa Sirro akianza na kilichotokea katika mchezo uliopita kati ya Simba na Yanga