Jumapili , 26th Feb , 2017

Kocha mwenye maneno mengi ambaye hivi karibuni alitangaza kustaafu kufundisha mpira nchini Jamhuri Kihwelo 'Julio' ameibuka na kuiponda Yanga kuwa haikuwa na uwezo wa kuifunga Simba, huku akiifananisha na gari ya maiti

Julio ambaye amewahi kuichezea Simba na baadaye kuifundisha kwa nyakati tofauti, ametoa kauli hiyo mara baada ya Simba kuishushia kipigo Yanga cha mabao 2-1 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa katika dimba la Taifa Dar es Salaam.

Kocha huyo ambaye alitangaza kustaafu akiwa na timu ya Mwadui FC kwa madai ya kuchoshwa na waamuzi wa Tanzania, amesema ameamua kuunganisha nguvu kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa zamani wa Simba akiwemo Zamoyoni Mogella, kuunda kundi la hamasa kwa wachezaji wa Simba ili kuhakikiksha Simba inaifunga Yanga na kuchukukua ubingwa msimu huu.

Amesema kabla na wakati wa mchezo wa jana, yeye na wenzake wamefanya kazi kubwa ya kuwatia hamasa wachezaji na hata wakati wa mapumziko, waliingia vyumbani na kuwatia hamasa wachezaji ya kupambana na ndiyo maana timu kipindi cha pili ilibadilika na kucheza kwa ari kubwa.

Mashabiki wa Yanga wakiwa wamekaa kwa huzuni mara baada ya timu yao kupigwa bao 2-1 na timu ya Simba katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania bara

"Sisi kazi yetu ni kuwahamasisha wachezaji, hatumuingilii mwalimu, mwalimu anafanya kazi yake, lakini sisi tunawaambia wachezaji wanapaswa kupambana, ndiyo kazi tuliyoamua kuifanya kuelekea mchezo huu hata wakati wa mapumziko, kwa kazi tuliyofanya Yanga wasingeweza kutufunga, na mimi tangu nimeanza kufundisha mpira sijawahi kufungwa na Yanga, .. Yanga ni kama gari ya maiti, ya kwanza kuondoka, ya mwisho kurudi, ndiyo maana nasema hawa ni kama mwembe wetu wa uwani, wakati wowote tunautikisa unadodosha maembe" Amesema Julio.

Pia Julio amewapongeza makocha wa Simba kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuusoma mchezo na kufanya mabadiliko yenye tija, pamoja na kuwajenga wachezaji kisaikolojia, ambapo licha ya kuwa nyuma, pamoja na mchezaji wao mmoja kutolewa, walionesha kutokata tamaa.

Wachezaji wa Simba wakishangilia bao la kusawadhisha liliwekwa kimyani na mshambuliaji Laudit Mavugo