Jumatano , 29th Mar , 2017

Msanii Jacob Stephen maarufu kama JB amefunguka na kusema klabu ya Yanga ni chanzo cha watu wengi kupatwa na matatizo ya moyo ambayo hupelekea vifo kwa sababu klabu hiyo haina furaha wala haiwapi furaha mashabiki wake ukifananisha na klabu ya Simba.

JB

JB alisema hayo kupitia katika kipindi cha KIKAANGONI kinachorushwa kupitia ukurasa wa facebook wa EATV na kusema toka ameifahamu Simba akiwa mtoto mdogo imekuwa ni klabu ambayo inampa furaha muda mwingi.

Amesema timu ya Yanga haiwezi kuwa ya kimataifa kutokana na historia yake ya michezo inayoonesha kutolewa katika baadhi ya mashindano ya kimataifa mara kwa mara.

"Watani zetu wa jadi wanaongoza kwa kuua watu maana wanafungwa kila mara ila mimi binafsi huwa nafurahi sana nikiona wanafungwa na hata kama nikiwa kwenye hasira zangu, mke wangu akija akinionesha video zinaonesha wanavyofungwa huwa 'automatical' nacheka". Alisema JB

Akizungumzia chimbuko la yeye kuanza kushabikia Simba, JB anasema

"Mimi kushabikia Simba ni kama nimerithishwa na baba yangu, nakumbuka wakati nipo mdogo tulikwenda uwanjani na siku hiyo Simba ilishinda bao 6, nikajikuta naipenda ile timu na nilipomwambia baba yangu aliniambia ukitaka furaha siku zote kuwa Simba. Yanga ni klabu kubwa Afrika na imebahatika kuchukua ubingwa mara kadhaa, ila aina ya mpira wa Yanga hainifurahishi ila ni klabu ambayo imesababisha watu wengi kupata magonjwa ya moyo, hivyo Yanga hakuna furaha" alisema JB 

Kichuya

JB anasema kama mwaka huu Simba haitachukua ubingwa yeye ataumia sana na kulia kabisa 

"Kiukweli Kichuya aliniliza kwa furaha maana goli aliloifunga Yanga siku zile lilikuwa ni goli la ajabu sana, sikutegemea kabisaa kupata goli tukiwa 10 uwanjani hivyo siku zile nililia kwa furaha. Lakini pia wachezaji wananifahamu vizuri wasipofanya vizuri huwa nawapigia simu nawatukana sana tu, maana namba za wachezaji wote wa Simba ninazo hivyo wananijua" alisema JB 

Mbali na hilo JB anadai katika vitu ambavyo huwa vinamfurahisha sana katika maisha yake ni kumfunga Yanga tena wakati timu yake Simba ikiwa pungufu uwanjani.

"Vipo vitu vitatu ambavyo mimi napenda moja ni kwenda mbinguni, mbili ni kuishi maisha matakatifu na cha tatu ni kumfunga Yanga ni kitu ambacho napenda sana kuna muda mwingine naweza kuboreka lakini nikiangalia magoli ya Kichuya nabaki na tabasamu. Hata mke wangu analijua hilo saizi akiona nimenuna tu anaweka yale magoli yaani najikuta na furaha ya ajabu na kuanza kutabasamu" alisisitiza JB 

Vile vile JB amesema katika wachezaji wote wa kikosi cha Yanga anampenda zaidi Saimo Msuva kwa kuwa anaujua vizuri mpira na kumshauri ajiunge na Simba ili aweze kupata furaha ya moyo wake.

Msuva