Jumapili , 15th Jan , 2017

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Yanga SC wanaondoka leo kwenda Songea tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu siku ya Jumanne katika dimba la Majimaji Songea huku ikiacha wachezaji 7 kwa sababu tofauti.

Donald Ngoma

Mshambuliaji hatari wa timu hiyo Mzimbabwe Donald Ngoma na Wazambia Justin Zulu na Obrey Chirwa ni kati ya wachezaji saba ambao hawatakuwamo safarini.

Kaimu katibu mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit amesema kwamba watatu hao wote bado ni majeruhi na wanaendelea na matibabu.

Baraka amesema kwamba winga Emmanuel Martin yeye hatakuwamo safarini kwa sababu yuko kwenye msiba wa mdogo wake  jijini Tanga, huku Vincent Bossou yupo na timu yake ya taifa, Togo kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Gabon, wakati mshambuliaji Malimi Busungu anaachwa kwa sababu hayupo fiti. 

Kwa mujibu wa Baraka benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina linataraji kuondoka na kikosi cha wachezaji 20 tu kwenye mchezo huo kikiongozwa na makipa; Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Pato Ngonyani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan.

Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Juma Mahadhi, Deus Kaseke, Simon Msuva, Yussuf Mhilu, Geoffrey Mwashiuya na washambuliaji Amissi Tambwe na Matheo Anthony.