Jumatano , 29th Mar , 2017

Mabingwa watetezi wa Tanzania Bara Yanga wamesema mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Kati yao na MC Alger ya Algeria utachezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam badala ya CCM Kirumba Mwanza

Kikosi cha Yanga

Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amesema,kutokana na hali halisi ya Uwanja ikiwemo marekebisho yanayotakiwa kufanyika kabla ya mchezo huo utakaopigwa Aprili 08 mwaka huu wameamua mchezo huo uchezwe jijini Dar es salaam huku akiongeza kuwa watahakikisha wanajipanga ili kuweza kuwapelekea mashabiki wao baadhi ya mechi za kimataifa jijini Mwanza.

Amesema lengo la wao kutaka kuchezea uwanja wa CCM Kirumba lilikuwa ni kutaka kuwapa fursa mashabiki wa kanda ya ziwa nao wapate kuona hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. 

"Ni kweli tulipanga tukachezee Mwanza hatukuwa na lengo la kuwakimbia mashabiki wa Dar es salaam kwa kuwa hata huko tunao mashabiki hivyo tukataka watu wote wapate haki sawa isipokuwa tulitaka kubadilisha tu upepo na watu wengine wapate fursa, Yanga popote pale inaweza kucheza kwa kuwa ina 'funbase' kubwa". Alisema Mkwasa

Wakati huohuo Mkwasa amesema kikosi cha Yanga kimeingia kambini hii leo mara baada ya kumaliza mazoezi ya jioni kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam FC ikiwa ni muendelezo wa Michuano ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.