Jumanne , 26th Jul , 2016

Klabu ya Yanga ya Dar es salaam Tanzania leo imejiweka katika mazingira magumu zaidi ya kufuzu kuingia katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya kuchapwa bao 3-1 na Medeama ya nchini Ghana.

Mshambuliaji wa Yanga (Amiss Tambwe (Kushoto) akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa Medeama

Mechi hiyo iliyopigwa katika dimba la Essipong Sports, imeshuhudia Yanga Ikionesha kandanda lisilo na matumaini, na kuwaruhusu wapinzani wao kutawala sehemu kubwa ya mchezo kwa kufanya mashambulizi yenye uhai zaidi.

Medeama wamefungua kitabu chao cha mabao mapema kabisa kwa kosakosa moja dakika ya 5 kabla ya kupata bao lao la kwanza kati ya dakika ya 7 kupitia kwa Daniel Amoah.

Yanga imeendelea kushambuliwa mashambulizi ambayo yalizaa penati kwa Medema, ambayo hata hivyo, Medeama walishindwa kuitumia vizuri penati hiyo ambayo iliokolewa kiustadi mkubwa na golikipa namba moja wa Yanga Deogratius Munis Dida, kabla ya kupata bao la pili kupitia kwa Abbas Mohammed dakika ya 23.

Yanga ilizinduka na kufanya mashambulizi yaliyozaa penati iliyotokana na mshambuliaji wa Yanga Chirwa kuangushwa katika eneo la hatari, na penati hiyo kufungwa kiufundi na Simon Msuva dakika ya 25.

Medeama walicharuka na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara yaliyozaa bao la tatu dakika ya 36, kupitia kwa Abbas Mohammed tena na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Medeama ilikuwa inaongoza kwa mabao 3-1.

Matokeo hayo hayakubalika hadi dakika 90 zinamalizika, licha ya timu zote kuonesha uwezo wa mashambulizi ya hapa na pale.

Mechi hii ni ya marudiano ambapo katika mchezo wa kwanza kati ya Yanga na Medeama uliopigwa katika dimba la Taifa Dar es salaam, timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1.

Kwa matokeo haya, Yanga inabaki na pointi yake 1 katika Kundi A, huku Medeama wakifikisha pointi 5 sawa na MO Bejaia, huku TP Mazembe ikongoza kwa kuwa na pointi 7.

TP Mazemba na MO Bejaia wanakutana kesho nchini DRC.