Ijumaa , 1st Jul , 2022

Uongozi wa klabu ya Azam FC imeendelea kushusha vifaa, baada ya kumtangaza mchezaji watatu wa Kimataifa, ikiwa ni muendelezo wa usajili kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa msimu wa 2022/23.

Mabosi wa Azam FC wakiwa kiungo mkabaji, Isah Ndala kutoka Plateau United ya kwao, Nigeria

Timu hiyo leo imemtangaza kiungo kutoka nchini Nigeria Isah Ndala, ambaye aliwahi kuja Tanzania na klabu ya Plateu United iliyocheza na Simba katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2019/20.

Ndala alionyesha uwezo mkubwa katika michezo yote dhidi ya Simba SC, na kuibua gumzo kubwa miongoni mwa wadau wa soka, huku Simba wakihusishwa kutaka huduma za kiungo.

Azam imethibitisha kukamilisha usajili wa kiungo huyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ikiandika: Tumefanikiwa kunasa saini ya kiungo mkabaji kutoka Nigeria, Isah Ndala, tukiingia naye mkataba wa miaka miwili.

Huo unakuwa ni usajili  wa tatu kuelekea msimu ujao, baada ya jana kuwatangaza nyota wawili kutoka Ivory Coast, Kipre Junior na Tape Edinho.