Alhamisi , 30th Jun , 2022

Uongozi wa Klabu ya Yanga umethibitisha kuwa nyota wake Fiston Mayele hawezi kuondoka klabuni hapo kwasababu bado ana mkabata mrefu na Mabingwa hao wa Ligi Kuu NBC Tanzania msimu huu wa mwaka 2021-2022.

Straika wa Yanga Fiston Mayele

Maneno hayo yamethibitishwa na Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo Senzo Mazingiza ambaye amesema taarifa zilizoripotiwa kuwa nyota huyo ameuzwa kwenda klabu ya Kaizer Chiefs ni za uongo huku akisema, endapo Mayele ataondoka na yeye yupo tayari kuondoka Yanga.

"Hizo ni taarifa za uongo huku ndani kwetu hakuna kitu cha namna hiyo, nilishatoa msimamo wa klabu kwamba Mayele hauzwi kwa gharama yoyote," amesema Senzo.

Aidha Senzo ameongeza kwamba kwasasa mshambuliaji huyo aliyemaliza wa pili katika ufungaji wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 16, akili yake inajiandaa na mchezo wa Fainali ya Azam Shirikisho dhidi ya Coastal Union itakayopigwa Julai 2 jijini Arusha.

Naye mtoto wa mmiliki wa klabu ya Kaizer Chiefs Kaizer, Motaung Junior amekanusha taarifa hizo kupitia akaunti yake ya Twitter akiandika kwa kifupi "msimu wa habari za kipuuzi unaendelea".