Wenyeji wa Moshi wakitazama na kusherekea tamasha la Kili Music Tour 2014.

TAMASHA la kwanza linalohusisha ziara ya wanamuziki zaidi ya 10 linalodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, limeanza kwa kishindo mwishoni mwa wiki ambako zaidi ya wakazi 10,000 walihudhuria na kusababisha msisimko mkubwa kwa wasanii waliotumbuiza tamasha hilo kwenye Uwanja wa Muccobs mjini hapa.

Tamasha la Moshi, ambalo lilikuwa la aina yake, zilizojaa shangwe na msisimko mkubwa, lilifunguliwa na kundi maarufu la Reggae mkoani Kilimanjaro, Warriors From The East na kufuatiwa na mwanamuziki aliyejizolea umaarufu mkubwa siku za hivi karibuni, maarufu kwa jina la Young Killer.

Profesa Jay alithibitisha kwamba kuwepo kwake ndani ya medani ya muziki wa kizazi kipya kwa muda mrefu, kunaweza kuwa sababu ya msingi ya kumkusanyia mashabiki wa rika zote, baada ya kupanda kwenye jukwaa na kupokelewa na kelele za mashabiki ambazo zilimpa hamasa na kufanya onesho la dakika 40 zenye mvuto na shamra shamra.

AY naye alichangamsha pale alipoibuka katikati ya onesho hilo kumsindikiza swahiba wake MwanaFA na kuibua shangwe zilizosababisha mwanamuziki huyo kulazimika kuimba wimbo wake binafsi mmoja na kisha kumuacha Mwana FA akimalizia ngwe yake na wimbo wake mpya aliomshirikisha G Nako ulio maarufu kwa jina la Mfalme.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, ambaye alihudhuria tamasha hilo, alisema, mwaka jana Moshi iliweka rekodi ya kuwa na watu wengi zaidi na mwaka huu pia wameonesha kuwa, wanapenda burudani na pia wameonesha uzalendo mkubwa kwa wasanii waliotoa burudani, kwani kila msanii alishangiliwa kwa nguvu muda wote.

Ziara hii inayoratibiwa na kampuni ya EATV, East Africa Radio, Executive Solutions, Integrated Communications na AIM Group, sio ya washindi wa tuzo za muziki, Kili Music Awards, bali inahusisha wasanii mbalimbali na lengo ni kuwasaidia kuwafikia wananchi wa mikoani ili kutangaza kazi zao na pia kutoa burudani.

Baada ya kutoka Moshi, ziara hii itaelekea Mwanza Mei 31, Kahama Juni 7, Songea Juni 14, Iringa Juni 21, Mbeya Agosti 9, Dodoma Agosti 16, Tanga Agosti 23, Mtwara Agosti 30 na Dar es Salaam Septemba 6.