Jumanne , 7th Aug , 2018

Bei za mafuta ya Petroli, Dizeli na mafuta ya meli visiwani Zanzibar zimeshuka huku bei ya mafuta ya taa ikitajwa kupanda kwa asilimia 4 mwezi Agosti na kufikia kuuzwa shilingi 1,854 kwa lita.

Kituo cha kutolea huduma ya mafuta

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha uhusiano kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji Zanzibar (ZURA), Khuzaimat Bakar na wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari na kusema bei hizo mpya zitaanza kutumika rasmi leo Agosti 07, 2018 katika vituo vyote vya kuuzia mafuta visiwani Zanzibar.

"Bei ya reja reja mafuta ya taa kwa mwezi wa Agosti, 2018 imepanda kwa shilingi 77 kwa lita kutoka shilingi 1,777 kwa lita mwezi Julai, 2018 hadi shilingi 1,854 katika mwezi wa Agosti sawa na asilimia 4. Mafuta ya Petrol kwa bei ya reja reja kwa mwezi Agosti yameshuka kwa shilingi 25 kwa lita kutoka shilingi 2,435 ya mwezi Julai, 2018 hadi shillingi 2,410 kwa lita mwezi Agosti, 2018 ambayo sawa na asilimia 1", amesema Khuzaimat.

Pamoja na hayo, Khuzaimat ameendelea kufafanua kuwa "bei ya reja reja ya dizeli kwa mwezi Agosti imeshuka kwa shilingi 35 kwa lita kutoka shilingi 2,430 ya mwezi Julai hadi shilingi 2395 sawa na asilimia 1.4".

Mbali na bei hizo, pia Khuzaimat amesema bei ya mafuta ya meli yameshuka kwa mwezi Agosti kwa shilingi 36 kwa lita kutoka shilingi 2,259 kwa lita katika mwezi Julai, 2018, hadi shilingi 2,222 katika mwezi Agosti sawa na asilimia
1.5.

Kushuka kwa baadhi ya bei hizo kunatokana mabadiliko ya mauzo ya mafuta hayo katika soko la dunia.

Bei ya Mafuta ya Petroli katika soko la dunia kwa mwezi wa Julai, 2018 imeshuka kwa shilingi 13 sawa na asilimia 1, bei ya mafuta ya Dizeli ikishuka kwa shilingi 33 sawa na asilimia 2.5, bei ya mafuta ya meli kushuka kwa shilingi 33 sawa na asilimia 2.5  huku bei ya mafuta ya taa yakiwa yamepanda kwa shilingi 107 sawa na asilimia 9.