Precision Air kuanza safari zake za Mbeya

Ijumaa , 27th Mar , 2020

Shirika la ndege la Precision Air limetangaza kurejesha rasmi safari zake za ndege mkoani Mbeya, kupitia uwanja wa Ndege wa Songwe, huku lengo likiwa ni kuhakikisha linaiunganisha Tanzania katika utoaji wa huduma wa usafiri wa anga.

Ndege ya Precision Air

Taarifa hiyo imetolewa na Meneja Mahusiano wa shirika hilo Hillary Mremi, ambaye amesema kuwa safari hizo zitaanza mapema mwa mwezi Aprili mwaka huu na kwamba nauli zake ni nafuu ambazo zitamuwezesha mteja wake kupunguza gharama kwa ajili ya mahitaji mengine.

"Kuanzia Aprili 6 kutakuwa na safari za ndege za kila siku kwenda Songwe, ambayo ndege itatoka Dar es Salaam saa 3:40 asubuhi na itawasili Mbeya saa 5:30 asubuhi, na itageuza tena na kuwasili Dar es Salaam 7:50 mchana, tunafarijika kurejesha tena safari zetu"ameeleza Mremi.

Aidha katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana kukabiliana na ugonjwa hatari unaosababishwa na Virusi vya Corona, shirika limekwishachukua tahadhari mbalimbali, ikiwemo kuhakikisha uwepo wa upatikanaji wa vitakasa mikono (hand sanitizers) kwa ajili ya abiria na wahudumu wa ndege.