TRA yakusanya Trilioni 3.84, maombi 1950 yatajwa

Jumatatu , 8th Oct , 2018

Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), imekusanya kiasi cha jumla ya shilingi trilioni 3.84 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 sawa na ukuaji wa asilimia 5.32% ndani ya miezi 3, ikilinganishwa na shilingi trilioni 3.65 zilizokusanywa kipindi cha miezi hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Elimu na huduma kwa mlipa kodi TRA, Bw. Richard Kayombo amesema fedha hizo zilizokusanywa zimetokana na ongezeko la walipakodi nchini, ndani ya kipindi cha mwezi Julai, Agosti na Septemba mwaka huu.

"Katika mwezi Julai tulikusanya trilioni 1.2 sawa na 9.2%, Agosti tulikusanya trilioni 1.27 sawa na 5.86% na Septemba tulikusanya trilioni 1.36 sawa na 1.65%, kodi zote hizi zimetokana na kuongezeka kwa walipa kodi, kulipa kodi kwa hiari kote nchini, kwani kama TRA tumekuwa tukiendelea na juhudi za kuhakikisha elimu ya ulipaji kodi inawafikia wananchi." amesema Kayombo.

Aidha akitoa takwimu juu ya zoezi la kutoa msamaha wa riba na adhabu kwa wale wanaostahili kwa malimbikizo ya kodi za nyuma Bw. Kayombo amesema, "mpaka sasa tumepokea maombi 1950 kwa walipa kodi kote nchini yanayojumuisha riba na adhabu ya shilingi bilioni 185.4, ambapo maombi mengi yamejibiwa huku tukiendelea kuyafanyia uvumbuzi yale ambayo yamebaki na tunawaomba walipa kodi wajitokeze kwani mwisho wa zoezi hili ni Novemba 30, mwaka huu".

Pia Kayombo amewaonya wale wote wanaofanya udanganyifu katika risiti za 'EFD' kuacha kugushi na kutoa risiti zisizo halali, huku akisema tabia hiyo imesheheni maeneo ya biashara mitaa ya Kariakoo, jijini Dar es salaam na kuahidi kuwafikisha mahakamani wale wote watakaobainika na uvunjaji wa sheria hiyo.