Jumanne , 12th Feb , 2019

Serikali ya Mkoa wa Iringa imetangaza kuwasaka wafanyabiashara wa mitandaoni kama moja ya mkakati wake hadi Mei 7, mwaka huu, unaolenga kila anayefanya biashara mkoani humo alipe kodi au awe na kitambulisho cha machinga.

Mkakati huo umetangazwa na  Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi baada ya kupokea taarifa ya ugawaji wa vitambulisho 25,000 vya awali vya machinga katika hafla iliyohusisha ugawaji wa nyongeza ya vitambulisho vingine 35,000 kwa halmashauri tano za mkoa huo.

Taarifa hiyo inaonesha tangu vitambulisho hivyo vya awali 25,000 vianze kugaiwa kwa Sh 20,000 kwa wafanyabiashara ndogo wa halmashauri hizo Desemba mwaka jana, vitambulisho zaidi ya 9,000 vilikuwa vimeshachukuliwa hadi wiki iliyopita.

Ndani ya mkoa wa Iringa hatutaki kuwa na mjasiriamali ambaye hayupo katika moja kati ya mifumo mitatu inayoiwezesha serikali kuwatambua", amesema Hapi.

Alisema anayefanya biashara bila kuwa na moja kati ya vitu hivyo vitatu, huyo hana tofauti na mhujumu uchumi na ni lazima atafutwe ili afuate utaratibu.

Wanauza nguo, keki, vyakula, bidhaa za tiba za jadi na biashara yoyote ile mkoani kwetu kupitia mitandao ya kijamii, katika simu za mikononi na vifaa vingine vinavyotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano, watatafutwa ili wasajiliwe katika moja ya mifumo hiyo", ameongeza Hapi.