Jumamosi , 21st Jul , 2018

Klabu ya Simba kupitia kwa kaimu Makamu wake wa Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ imesema kuwa haiwezi kusajili mchezaji yoyote kutoka klabu ya Yanga kwa sasa kwakuwa inafahamu hali ngumu inayoikumba klabu hiyo.

Wachezaji wa Simba na Yanga wakiwa katika hali ya ushindi.

Inafahamika kuwa siku za karibuni kumekuwa na tetesi za Simba kutaka kumsajili mchezaji Kelvin Yondani kutoka kwa mahasimu wao baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu uliokwisha.

Baada ya tetesi hizo kusambaa ndipo uongozi wa Yanga kupitia kwa Mwenyekiti wa kamati maalumu ya kuinusuru klabu hiyo, Abbas Tarimba walipokutana na Yondani na kumalizana naye kwaajili ya kuendelea kucheza msimu ujao.

Akizungumzia kuhusu tetesi hizo, Try Again amesema kuwa Yondani ni mchezaji Tegemeo wa Yanga na endapo Simba ikimsajili manaake wataibomoa klabu hiyo na itakuwa haijengi mpira wa Tanzania akilinganisha na usajili wa msimu uliokwisha wa Haruna Niyonzima na Ibrahim Ajibu kwa klabu hizo.

Tunafahamu Yanga wako kwenye matatizo, na hali ngumu sasa tunapoendelea kuwabomoa hatuusaidii mpira bali tunaudidimiza mpira “. Amesema Salim Abdallah

Msimu uliopita klabu ya Simba ilimsajili Haruna Niyonzima kutoka Yanga na Yanga ilimsajili Ibrahim Ajibu kutoka Simba wakiwa na mategemeo makubwa ya kufanya vizuri katika ligi lakini wachezaji hao wakuweza kuzisaidia klabu zao kwa kiwango ambacho kilitarajiwa.

Ajib alimaliza msimu akiwa na magoli 7 pekee huku Haruna Niyonzima akicheza katika mzunguko wa kwanza wa ligi pekee baada ya kuumia katika mzunguko wa pili.