Ijumaa , 22nd Jun , 2018

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema kuwa uhalifu upo kila mahali na si wa kutumia silaha tu kama watu walivyokariri, na kusema kuwa ulinzi unaimarishwa kila pande.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro akizungumza na wananchi wa Kibiti alipokuwa katika ziara yake ya kutoa elimu kwa raia wa eneo hilo.

Kamanda Sirro amefunguka hayo kwenye East Africa Drive, ya East Africa Radio ambapo amesema kuwa jeshi la polisi limekuwa likiendesha oparesheni mbalimbali na uhalifu sio wa kutumia tu silaha bali kila sekta inatakiwa kupewa uangalizi.

“Uhalifu haulipi na sio kwamba upo wa kutumia silaha tu, bali kila idara una namna yake ya kukabiliana na uhalifu, ili kuhakikisha hali ni shwari kila mahali”, amesema Kamanda Sirro.

Aidha Kamanda Sirro ameongeza kuwa bado wanaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa wananchi wa Kibiti, ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeingia kinyume na sheria na endapo wakiona mgeni ambaye hawamuelewi waripoti katika vyombo vya dola.