Jumamosi , 23rd Jun , 2018

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM) Prof. Anna Tibaijuka, amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango kutoa maelezo ya kutosha ya kuelezea ni kwa namna gani deni la Taifa ni himilivu wakati sehemu kubwa ya pato la ndani inakwenda kulipia deni hilo.

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM) Prof. Anna Tibaijuka

Prof. Tibajuka amesema hayo, Bungeni Jijini Dodoma, wakati wa kuchangia hoja kujadili hali ya uchumi na Mpango wa maendeleo ya Taifa, na kusema kuwa deni la Taifa mpaka sasa linachukua asilimia 49 ya pato ya ndani na kuongeza kuwa fedha hizo ni nyingi na hivyo inatia mashaka kama deni la Taifa linahimilika.

“Fedha nyingi zinapoenda kuhudumia deni, hapo uhimilivu unaanza kuwa wa mashaka, kwahiyo naomba Waziri utuletee majibu mazuri kutupa faraja kujua kwamba hili deni tumejisahau wapi, tunakopa zaidi, tunaendelea kutegemea kukopa, tunakusanya mapato ya ndani lakini yanaenda kwenye matumizi, maendeleo yatakwama kwasababu tunakopa” amesema Prof. Tibaijuka.

Mbunge huyo ameongeza kuwa ili kuleta maendeleo nchini, Serikali haina budi kupunguza kukopa mikopo yenye masharti ya kibiashara katika miradi ya mikubwa ya maendeleo na kuitaka kurudi kukopa katika mikopo yenye masharti nafuu.