Jumatatu , 11th Mar , 2019

Ikiwa ni masaa machache tu tangu ndege inayomilikiwa na shirika la ndege la Ethiopia aina ya Boeing 737 Max 8, kuanguka na kuua watu wote 157 walikuwemo, imebainika kuwa ndege ya aina hiyo ilianguka miezi mitano iliyopita na kuua watu wote 189 waliokuwemo.

Ndege hiyo ambayo ilikuwa inamilikiwa na shirika la ndege la Lion nchini Indonesia, ilianguka Oktoba 29, 2018 na kuua watu wote 189 waliokuwemo, na kupelekea kufananisha na ajali ya Boeing 737 Max 8 ya Ethiopia iliyotokea Machi 10, 2019

Ajali ya ndege ya Lion ilitokea dakika 13 tu baada ya kupaa kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Jakarta Indonesia, wakati ajali ya ndege ya Ethiopia imetokea dakika 6 baada ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Adis Ababa.

Ndege ya Lioni ambayo ni Boeing 737 Max 8 Ndege ya Lion ilipoanguka baharini na kuua watu 189

Usichokijua kuhusu Boeing 737 Max 8

Boeing 737 MAX ni ndege ya biashara inayotengenzwa na kampuni ya Boeing ya Marekani, ambao pia ni watengenezaji wa ndege ya Boeing 787 Dreamliner, iliyonunuliwa na Tanzania hivi karibuni.

Ndege ya Boeing MAX 8 ilianza kuingia sokoni kwa mara ya kwanza Mei 16, 2017, baada ya kununuliwa na Shirika hilo la Ndege la Lion linalofanya safari za ndani nchini Indonesia.

Ndege hizo ziliendelea kuuzwa kwa nchi mbalimbali, ambapo Ethiopa ilinunua yakwake mwaka 2018, na kuwa nchi ya kwanza Afrika kununua aina hiyo ya ndege.

Baada ya ajali hizi mbili za karibuni zilizotokea, utengenezaji wa ndege hizo umeanza kuzua wasiwasi miongoni mwa mashirika mengi ya anga duniani, ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Safari za Anga ya China imetangaza kusitisha kutumia ndege hizo.

Vile vile shirika la ndege la Ethiopia limetangaza kusitihsa kutumia ndege zake zote aina ya Boeing, ili kuchukua tahadhari zaidi baada ya ajali kutokea, ambayo mpaka sasa haijajulikana imesababishwa na nini.