Abdul Nondo amehukumiwa tayari - Lutembeka

Jumanne , 13th Mar , 2018

Katibu wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Taifa, Mhe. Rodrick Lutembeka amefunguka na kusema kuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ameshahukumiwa tayari kwa kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba. 

Lutembeka amedai kuwa wao kama baraza la wazee wa CHADEMA wamesikitishwa na kauli ya Waziri Mwigulu Nchemba juu ya sakata la kutekwa kwa kijana huyo kwa kusema kuwa amejiteka ili hali vyombo vya usalama wakiwepo polisi wao wamedai kuwa wanaendelea na uchunguzi wa sakata hilo. 

"Inasikitisha sana huyu kijana Abdul Nondo kama vijana wenzake walivyosema hakuonekana wakatoa taarifa polisi kwamba amepotea, ametekwa na wote tunafahamu hatimaye kijana huyo alikuja kuonekana Iringa na tunavyozungumza yupo mikononi mwa polisi lakini jambo ambalo limetuumiza sana sisi wazee wote kama mlifuatilia kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani akizungumza mbele ya Rais akisema kwamba kijana huyu alijiteka tena alisema kwa kebehi kubwa sana anasema alibeba mkoba, perfume, aliweka nguo za kubadilisha, inaumiza sana katika nchi ambayo ina utawala bora waziri mwenye dhamana ambaye alituhumiwa na hao vijana kwamba anapaswa kujiuzulu kwa kutochukua hatua baada ya kifo cha mwanafunzi mwenzao sasa waziri huyu huyu anatamka maneno haya mbele ya Rais" 

Lutembeka aliendelea kusema kuwa 

"Wote tunafahamu vyombo vya serikali yaani polisi imetueleza wazi kwamba wanaendelea kufanya upelelezi, yaani wanapeleleza juu ya kutekwa kwa kijana huyu sasa kama waziri muhusika anayesimamia wizara inayohusika na hao polisi amekwisha kutoa hukumu kwamba kijana huyu amejiteka, tunatizamia nini tena kutoka kwa vyombo vilivyo chini yake ambavyo ni polisi, jambo hili linatuumiza na sisi kama wazee kinachotuumiza zaidi tunaumba jambo gani ndani ya mioyo ya vijana hawa kama siyo uchungu, chuki juu ya taifa lao"