'Acheni kiherehere' - Rais Magufuli

Alhamisi , 11th Apr , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wanafunzi waliopo mashuleni kuachana na tabia ambazo zitawafanya washindwe kumaliza masomo yao kutokana na sababu ya kupata mimba.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Ametoa kauli hiyo akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Njombe wakati akizungumza na baadhi ya wanafunzi ambao walijitokeza kwenye ziara yake.

Rais Magufuli amesema, "na nyinyi watoto muache viherehere nawaambia ukweli wanangu, mtu anakwambia ninakupandisha pikipiki, acheni viheherere wewe kama bado ni mdogo tulia kwanza utavikuta, utavikimbia mwenyewe na utavichoka, pata elimu yako kwanza utakuja kumchagua unayemtaka."

"Mtu akikutongoza anakufuatilia sana mpeleke kwa Mkuu wa Mkoa wa Mkuu wa Wilaya sema huyu kila siku ananitongoza.", ameongeza Rais Magufuli.

Rais Magufuli kwa sasa anafanya ziara mkoani Njombe ambapo atazindua miradi mbalimbali, ikiwemo ya barabara pamoja na ujenzi wa hospitali.