Alhamisi , 23rd Jan , 2020

Mamlaka ya Mapato nchini Uganda (URA), imemkamata Duach Toang, Raia wa Sudan Kusini, akiwa na karatasi zenye usawa wa dola na kemikali ambayo ukiimwaga, karatasi hizo hubadilika na kuwa dola ambazo ni bandia.

Mtuhumiwa Duach Toang, na karatasi bandia zinazobadilika kuwa dola.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo imeeleza kuwa Duach alikamatwa wakati akivuka mpaka wa Malaba, akitokea nchini Kenya kupitia Uganda na kisha kuelekea nchini Sudan Kusini, wakati akifanyiwa ukaguzi wa mwili wake pamoja na mizigo yake ya mikononi.

"Ukitazama kwa macho ya kawaida utaona ni karatasi tu, lakini kwa kutumia kemikali iliyomo kwenye mzigo wa Duach, karatasi zilibadilishwa kuwa dola bandia, mtuhumiwa Duach alikamatwa na atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazomkabili" imeeleza taarifa hiyo.

Teknolojia yenye jina la (NII), iliyowekwa na mamlaka hiyo kwa lengo la kubaini vitu bandia, imekuwa ikiwaweka katika wakati mgumu wasafirishaji wa bidhaa hizo, kupitia mipaka nchini Uganda.