Alhamisi , 18th Feb , 2021

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefungua jalada la uchunguzi kwa Hospitali ya Aga Khan ya jijini humo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba wanatozwa gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wa matatizo ya 'Pneumonia' yanayopelekea matatizo ya upumuaji.

Hospitali ya Aga Khan

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 18, 2021, na Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo SACP Lazaro Mambosasa, na kuongeza kuwa pia wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo pindi wanapofariki kumekuwa na tabia ya kuzuia miili ya marehemu na kudai kiasi kikubwa cha fedha kinyume na maelekezo ya serikali.

Aidha SACP Mambosasa, ameongeza kuwa uchunguzi huo utakapokamilika na kubaini tuhuma hizi ni za kweli hatua kali za kisheria zitachukuliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto dhidi ya Hospitali hiyo.