Ahadi ya RC Makonda kwa kijana Hamis

Ijumaa , 15th Mar , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda leo amemtembelea na kumjulia hali kijana Hamis Hashim aliyelazwa katika Hospital ya Taifa Muhimbili akisumbuliwa na tatizo la miguu kuvimba hadi kuzidi uzito wa mwili, ambapo ameahidi kusaidia gharama za matibabu iwe ndani au nje ya nchi.

Paul Makonda akimjulia hali kijana Hamis, hospitali ya taifa Muhimbili.

Aidha RC Makonda amesema kwa sasa hali ya Afya ya Hamis inaendelea vizuri baada ya madaktari bingwa wa Muhimbili kuendelea kuchukuwa vipimo kwa umakini wa hali ya juu. Pamoja na hayo RC Makonda amemkabidhi Kijana Hamis kiasi cha shilingi laki tano kwaajili ya kununua chakula kwa siku atakazokuwa Hospital.

Kwa upande wake Hamis Hashim amemshukuru RC Makonda kwa moyo wa huruma aliokuwa nao ambapo ameeleza kuwa amekuwa anaishi maisha ya tabu lakini kwa sasa anajisikia faraja kuona RC Makonda ameahidi kumsaidia kwa kila jambo.

Kwa Mujibu wa Dr. Ibrahim Nkoma ambaye ni Mkuu wa idara ya upasuaji hospital ya taifa Muhimbili anasema Hamis Hashim anasumbuliwa na tatizo la neva za fahamu kukuwa kupita uwezo.

RC Makonda baada kuona taarifa za kijana Hamis kapitia mitandao ya kijamii aliguswa na juzi aliagiza apelekwe hospital kwaajili ya kuchukuliwa vipimo ambapo licha ya Hamis kuugua pia anaishi katika Familia ya hali ya chini akimtegemea Mama mzazi ambaye naye hana kazi baada ya Baba mzazi kufariki.