Jumatatu , 4th Nov , 2019

Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), limekamata mifuko ya plastiki yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 70, iliyokuwa ikisafirishwa kutoka Uganda na kuingia nchini kwa njia ambazo si halali.

Shehena ya mifuko ya plastiki ilikuwa ikiingia nchini kwa kutumia Bandari Bubu, iliyopo eneo la Bwiru Bombani wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, ambapo imetiwa hatiani kutokana na Serikali hivi karibuni kuweka katazo la kutumia mifuko hiyo.

Akizungumza na waandishi habari jijini Mwanza, Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa, Redemta Samwel, amesema mfanyabiashara aliyekamatwa na mifuko hiyo anafahamika kwa jina moja la Criss, na hivi karibuni atachukuliwa adhabu kali.

"Niendelee kuwakumbusha wananchi kutumia mifuko ambayo imepigwa marufuku ni kosa kwa hiyo niwaaambie tu jifunzeni kufuata sheria ili kuepukana na adhabu kali zinazotolewa" amesema Redemta Samwel.