Alhamisi , 6th Aug , 2020

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Dkt Bashiru Ally, amesema kuwa CCM haifanyi kazi na Bata kwa kuwa Bata ni wachafu, bali chama hicho kinafanyakazi na Watanzania na kwamba kinao uhakika wakushinda maeneo yote na hata Urais wa Zanzibar kitaupata mapema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Dkt Bashiru Ally.

Dkt Bashiru ametoa kauli hiyo hii leo Agosti 6, 2020, wakati akizungumza na wanachama wa CCM katika ofisi za chama hicho Dodoma, mara baada ya kumpokea mgombea Urais wa chama hicho Dkt Magufuli alipotoka kuchukua fomu za ugombea wa Urais kwenye ofisi za NEC.

"Mwaka huu tutasikia mengi, na tutakuwa na wagombea wa aina nyingi na tutapata misamiati ya kila namna na nimesikia msamiati wa Kazi na Bata, sasa sijui wanafanya kazi wakiwa na Bata, wakichinja Bata, wakilala na Bata au wanafanya kazi wakitumikisha Bata hilo nawaachia nyie" amesema Dkt Bashiru.

Aidha Dkt Bashiru ameongeza kuwa, "CCM si chama cha kufanyakazi na Bata, tena Bata ni wachafu usipokuwa makini, chama kinafanyakazi na Watanzania, kuna msemo kwamba eti Utapigiwa kura na Madaraja, Ndege na vivuko, Mahospitali na mashule, umeme wa vijijini na maji, watu watakupigia kura kwa sababu vitu hivyo umevifanya kwa jasho lao".