Jumatatu , 24th Feb , 2020

Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam imemuachia huru Mwandishi wa Habari za Uchunguzi Erick Kabendera na kumtaka kulipa fidia ya shilingi milioni 172, fedha ambazo anatakiwa kuzilipa ndani ya miezi sita.

Mwandishi wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera akiwa mahakamani.

Hukumu hiyo imesomwa leo Februari 24, 2020, ambapo ilimtaka mtuhumiwa kulipa kiasi cha shilingi 250,000 au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela, adhabu hiyo inaambatana na fidia ya Shilingi za kitanzania Milioni 172, kutokana na kosa la ukwepaji wa kodi.

Kosa la pili limemtaka Erick Kabendera kulipa faini ya shilingi Milioni 100, hii ikiwa ni adhabu kwa kosa la utakatishaji fedha katika kesi ya uhujumu uchumi, fedha ambayo tayari amekwishaiingiza kwenye akaunti ya Serikali.

Baada ya kuachiwa huru kabendera aliwashukuru wale wote waliosimama naye katika kipindi chote alipokuwa rumande.

"Binafsi niwashukuru wanataaluma wenzangu mliosimama na mimi kwa maombi na hata mliokuja kuniona Segerea, niwashukuru ndugu zangu wa karibu na marafiki zangu wa karibu hakuna kipindi ambacho nimeelewa umuhimu wa marafiki na ndugu kama hiki" amesema Kabendera.

Julai 29, 2019,zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii, zinazoeleza kuwa Erick Kabendera amekamatwa na watu wasiojulikana, nyumbani kwake maeneo ya Mbweni na Agosti 5 kwa mara ya kwanza alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka matatu ya uhujumu uchumi.