Alhamisi , 23rd Jan , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amemteua Meja Jenerali Jacob Kingu kuwa Balozi, kabla ya uteuzi Jenerali Kingu alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, mpaka jana Januari 22, 2020 ambapo aliandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo na akakubaliwa.

Meja Jenerali Jacob Kingu, aliyeteuliwa kuwa Balozi.

Uteuzi huo umetangazwa leo Januari 23, 2020 na Katibu Mkuu kiongozi Balozi Dkt John Kijazi, Ikulu ya Jijini Dar es salaam.

"Mabalozi walioteuliwa ni Meja Jenerali Jacob Kingu, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu jana Januari 22, 2020, mwingine ni Dkt John Steven Simbachawene, kutoka Ofisi ya Rais Ikulu pamoja na Kamishina Jenerali Phaustine Kasike, ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Kamishina Jenerali wa Magereza na nafasi yake itajazwa baadaye, vituo vya Mabalozi hao vitatangazwa baadaye" amesema Dkt Kijazi.

Uteuzi mwingine uliofamnyika leo ni pamoja na kumteua Mussa Zungu kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, akichukua nafasi ya George Simbachawene, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, akichukua nafasi ya Kangi Lugola.